Insulin: Dawa kwa ajili ya kutibu kisukari (Diabetes mellitus)
Kisukari ni ugonjwa ambao kimsingi hutokea pale ambapo mmeng’enyo wa wanga haufanyiki ipasanyo au kukamilika ipasavyo. Madhara ya muda mrefu ya kisukari ndio huwa chanzo kikubwa cha maradhi na vifo kama matibabu hayatafanyika kikamilifu.
Watu wanaougua kisukari husumbuliwa na magonjwa mengine kama vile magonjwa ya moyo na magonjwa ya mfumo wa mkojo kulinganisha na watu wengine, kisukari pia ndio sababu kuu ya watu wa magharibi kupata upofu.
Insulin
Insulin ni homoni ya asili inayozalishwa na kongosho katika mwili wa binadamu. Inafanya kazi kwa kusaidia seli za mwili kutumia sukari (glucose) iliyopo kwenye damu kwa ajili ya nishati. Insulin husaidia kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu kwa kuisaidia sukari kuingia ndani ya seli za mwili. Kwa watu wenye kisukari, kongosho haiwezi kuzalisha insulin ya kutosha au mwili hauwezi kutumia insulin vizuri, na hivyo wanahitaji sindano za insulin ili kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu.. Insulin hufanya kazi katika viungo kama vile:
Ini: Kwenye ini, insulin huongeza uwezo wa ini kuhifadhi sukari katika mfumo wa glycogen. Insulin pia katika ini hupunguza mmengenyo wa protini kwenda katika wanga.
Misuli ya uti wa mgongo: Insulin huamasisha kuzalishwa kwa glycogen na kutengenezwa kwa protini. Insulin pia huamasisha usafirishwaji wa sukari katika misuli.
Tishu za mafuta: Insulin huamasisha utunzaji wa mafuta, usafirrishaji wa sukari katika seli na kupunguza mmeng’enyo wa mafuta.
Dawa ya Insulin
Dawa ya insulin kwa binadamu huzalishwa kwakutumia teknolojia ambayo hujulikana kama Bacterial recombinant technology, ambapo inssulini huzalishwa kwa kutumia bacteria. Kwa kutumia teknolojia hii insulin tunapata aina nne za insulin ambazo huweza kufanya kazi kwa muda mrefu au kwa haraka.
Lengo la tiba hii ni kudhibiti sukari baada ya kula au wakati wowote ule bila kuzingatia chakula ili kuondoa hatari ya mgonjwa kupungukiwa na sukari mwilini.
Rapid-acting (Insulin ya haraka): Hujumuisha aina tatu za insulin ambapo zi insulin lispro, insulin aspart na insulin glulisine. Huanza kufanya kazi ndani ya dakika 10-15 baada ya sindano, na hufikia kiwango cha juu cha athari ndani ya saa moja. Hii mara nyingi hutumiwa kabla ya chakula.
Insulin ya haraka huchomwa mara tu kabla ya kula. Aina hii ya insulin hutumika wakati wa dharura kama mgonjwa atapata diabetic ketoacidosis. Hupendelewa kuchomwa katika ngozi.
Insulin ya kawaida (short-acting insulin): Huanza kufanya kazi ndani ya dakika 30-60 baada ya sindano, na athari yake huendelea kwa masaa 3-6. Hii hutumiwa kabla ya kula.
Insulin ya kati (intermediate-acting insulin): Huanza kufanya kazi baada ya saa 2-4 baada ya sindano, na athari yake huendelea kwa saa 12-18. Hii mara nyingi hutumiwa mara mbili kwa siku.
Insulin ya kuchelewa (long-acting insulin): Huanza kufanya kazi baada ya masaa 1-2 baada ya sindano, na athari yake huendelea kwa saa 24. Hii mara nyingi hutumiwa mara moja kwa siku.
Insulin ya mchanganyiko (mixed insulin): Hii ni mchanganyiko wa insulin ya kawaida na insulin ya kati. Inaweza kutumika mara mbili kwa siku.
Hatari ya kutumia insulin
Hypoglycemia: Hii ni hali ambayo viwango vya sukari kwenye damu hupungua sana. Dalili za hypoglycemia ni jasho, kutetemeka, kuchanganyikiwa, kizunguzungu, na njaa.
Kuongezeka uzito: Insulin inaweza kusababisha kuongezeka uzito, hasa kama haitumiwi kwa pamoja na lishe bora na mazoezi.
Athari kwenye eneo la sindano: Baadhi ya watu wanaweza kupata uvimbe, kuvimba au kuwashwa kwenye eneo la sindano.
Kutokea kwa mzio: Katika visa vichache, insulin inaweza kusababisha kutokea kwa mzio. Dalili za kutokea kwa mzio ni pamoja na vipele, kuwashwa, ugumu wa kupumua, na uvimbe kwenye uso, ulimi, au koo.
Lipodystrophy: Hii ni hali ambayo tishu ya mafuta chini ya ngozi inakuwa nene au nyembamba, ikisababisha vimbe au mashimo kwenye eneo la sindano.
Hypokalemia: Hii ni hali ambayo kiwango cha potasiamu kwenye damu kinapungua sana. Insulin inaweza kusababisha hypokalemia, ambayo inaweza kusababisha udhaifu wa misuli, kuchoka, na mapigo ya moyo yasiyo sawa.
Ni muhimu kuzungumza na daktari wako juu ya athari yoyote unayopata wakati unachukua insulin. Daktari wako anaweza kukusaidia kudhibiti athari hizi na kurekebisha matibabu yako kama inavyohitajika.
Ni watu gani wanastahili sindano ya insulin?
Watu wenye kisukari wanaweza kuhitaji sindano ya insulin ikiwa kongosho yao haitoi insulin ya kutosha au mwili wao hauwezi kutumia insulin vizuri. Hali hii inajulikana kama upungufu wa insulin au upinzani wa insulin. Watu wenye kisukari cha aina ya 1 hawawezi kuzalisha insulin ya kutosha na kwa hiyo wanahitaji sindano ya insulin kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. Watu wenye kisukari cha aina ya 2 wanaweza kuhitaji sindano ya insulin ikiwa lishe na mabadiliko ya mtindo wa maisha hayatoshi kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu, au kama dawa nyingine za kisukari hazifanyi kazi vizuri.
0 Comments