Kukoroma: sababu, athari na tiba-Ufafanuzi kamili

Kukoroma: sababu, athari na tiba-Ufafanuzi kamili

Kukoroma ni kitendo cha kupumua kwa sauti kubwa wakati umelala. Kukoroma ni hali ambayo inaweza kutokea kwa mtu yeyeote, wanaume huathirika zaidi kulinganisha na wanawake na hali huwa mbaya zaidi kadiri umri unavyo ongezeka.

Kukoroma hutokana na kutopata hewa ya kutosha (pumzi) wakati umelala. Wakati umelala, misuli ya mwili hupumzika, pamoja na tishu za koo na ulimi. Wakati huo tishu za koo huingia kwenye njia ya hewa na kuzuia mzunguko wa hewa. Hivyo, mtu hupumua kwa sauti kubwa, kitendo kijulikanacho kama kukoroma.

Unapo koroma wakati wa kulala, unaweza kuwa kero kwa mtu ambaye analala na wewe. Kukoroma si kwamba ni kero tu kwa wale ambao wanalala na wewe lakini pia kukoroma huaribu ubora wa usingizi wako.

Watu waliokatika hatari ya kupata tatizo hili ni pamoja na wale wenye uzito uliopindukia (overweight), uvutaji wa tumbaku, matumizi ya vilevi, matumizi ya dawa, tatizo la kiafya (sleep apnea).

Kukoroma: sababu, athari na tiba-Ufafanuzi kamili
"sleep apnea mask" by safoocat is licensed under CC BY-NC-ND 2.0. To view a copy of this licence, visit https://creativecommons.org/licenses/by-nd-nc/2.0/jp/?ref=openverse.


Apnea ya usingizi (sleep apnea)

Apnea ya usingizi ni tatizo la kiafya ambapo, kupumua husimama na kisha kuendelea wakati umelala usiku. Hali hii huweza kutokea mara nyingi na kusababisha mtu kuamka mara kwa mara bila kujua na kuathiri ubora wa usingizi.

Kuna aina kuu mbili za tatizo hili ambazo ni

  • Obstructive Sleep Apnea: Hii hutokea pale ambapo tishu za koo hulegea na kuziba njia ya hewa kupelekea mtu kukoroma.
  • Central Sleep Apnea: Hii hutokea pale ambapo ubongo hushindwa kutuma taarifa kwenye tishu inayohusika na kupumua wakati wa kulala.

Apnea ya usingizi huwa na athari kiafya kama vile

  • Kuchoka wakati wa mchana
  • Kusinzia mara kwa mara wakati wa asubuhi au mchana
  • Kukoroma kwa sauti kubwa
  • Kuamka katikati ya usiku mara kwa mara ukijihisi kupaliwa au kukabwa
  • Kuaka na kujihisi koo kukauka na vidonda vya koo
  • Kupungua kwa hamu ya kushiriki tendo la ndoa/kujamiiana
  • Kukosa muhamuko wa kihisisa (mood changes)
  • Kukosa umakini wakati wa chana
  • Uwezo wa kukumbuka na kutunza kumbukumbu kupungua
  • Maumivu ya kichwa wakati wa asubuhi.

 

Sababu zinazopelekea kukoroma

Njia ya hewa kuziba: Baadhi ya watu hukoroma kutokana na njia ya hewa kuziba kunakotokana na kuugua mafua, vinyama vya pua (nasal polyps), maambukizi katika vifuko vya hewa puani (sinus infection) na ukuta unaotenganisha pande matundu mawili ya pua kutokuwa sehemu yake ya kati (deviated septum).

Tishu za ulimi na koo kulegea: Tishu za koo na ulimi huweza kulegea na kuingia katika njia njia ya hewa na hivyo kupelekea kukoroma.

Uzito uliopindukia: Kwa baadhi ya watu wenye uzito uliopindukia huwa na mafuta mengi kwenye koo ambayo hupelekea kukoroma. Uzito mkubwa husababisha kuwa na tezi za tonsils kubwa ambazo pia husababisha kukoroma.

Uvutaji wa tumbaku/sigara: Uvutaji tumbaku husababisha njia ya hewa kuziba na kupelekea kukoroma

Matumizi ya pombe na dawa: Matumizi ya pombe na baadhi ya dawa hulegeza tishu za koo na kupelekea kukoroma.

Kulalia mgogo: Kulala chali kwa kulalia mgogo kunaweza kupelekea kukoroma

Kukosa usingizi: Misuli yako ya koo inaweza kulegea sana kama hupati usingizi wa kutosha.

Kutambua kama unakoroma

Kwa kawaida watu wengi hawatambui kama wanakoroma wanapokuwa wamelala. Mtu wako wa karibu ambaye hulala pamoja na wewe anaweza kukwambia iwapo unakoroma wakati wa kulala. Daktari anaweza kuwauliza wote kama kuna mmoja wenu anakoroma. Namna nyingine ya kujua kama unakoroma ni kwa kujichunguza kama unakumbana na athari zitokanazo na kukoroma kama vile kuchoka wakati wa mchana na vipindi virrfu vya kusinzia.

Kama hauna mtu anayeweza kukusaidia kukwambia kama unakoroma, unaweza kutumia programu za simu ambazo zinaweza kurekodi mwenendo wako wa usingizi na sauti ya kukoroma kwako.

Tabibu anaweza anaweza kuagiza vipimo ili kuangalia iwapo kuna sababu za kiafya zinazopelekea kukoroma kama vile, kuziba kwa njia ya hewa hutokana na mafua au mzio (allergy), uwepo wa vinyama vya pua au deviated septum na kuvimba kwa tezi za tonsils.

Vipimo vya picha kama CT-scan, X-ray na MRI-scan vinaweza kutumika kuangalia njia yako ya hewa.

Kuchunguza mwenendo wako wa usingizi kwa kutumia vifaa maalumu, vifaa hivi hurekodi mapigo ya moyo, ubongo na kupumua. Taaluma hii hujulikana kama polysomnography.

Tiba kwa mtu anaye koroma

  1. Kubadili mtindo wa maisha: Hii ni pamoja na kuepuka matumizi ya tumbaku, pombe, dawa za kulevya na kupunguza uzito kwa watu walio na uzito mkubwa.
  2. Kulala kwa upande. Kulala kwa upande badala ya kulala chali au kifudifudi inaweza kusaidia kuwa na mzunguko mzuri wa hewa na kuzuia kukoroma
  3. Matumizi ya vifaa vya kulalia: Vifaa kama vile vya kufungwa shingoni (snore guards) na mashine ya kupumulia (Continuous positive airway pressure-CPAP)
  4. Upasuaji: Tabibu wako anaweza kupendekeza kufanya upasuaji kuondoa tishu ambazo zinasababisha kukoroma.
  5. Kulalia mto
  6. Kupata masaa mengi ya kulala

Madhara yatokanayo na kukoroma

  • Kuamka mara kwa mara kutoka usingizini, japokuwa unaweza usitambue
  • Apnea ya usingizi huweza kusababisha shinikizo la juu la damu na kupelekea moyo kutanuka
  • Kukosa usingizi mnono.

 


Post a Comment

0 Comments